Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Habari

Itifaki ya AfCFTA ya Wanawake na Vijana itaondoa vikwazo wanavyokabiliana navyo kibiashara


Katibu Mkuu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamukele Mene amesema kuwa, mkutano wa wanawake na vijana katika biashara ni muhimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya vikao vya wakuu wa nchi na Serikali ya Umoja wa Afrika ambao waliazimia kupanua ushirikishwaji katika uendeshaji wa AfCFTA kupitia afua zinazosaidia vijana wa Afrika, wanawake na biashara ndogo na za kati (SMEs).

Mene ameyasema hayo katika wa sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya AFCFTA uliofunhuliwa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe  Samia Suluhu Hassan  Septemba 12, 2022 jijini Dar es salaam  

Amesema, sambamba na maagizo ya viongozi wa Afrika, Sekretarieti ya AfCFTA inafanya kazi ya maandalizi kuelekea katika hatua za kufanikisha Itifaki ya AfCFTA ya Wanawake na Vijana katika Biashara kuwaunganisha wafanyabiashara wasio rasmi wa mipakani katika uchumi rasmi kwa kutekeleza utaratibu wa biashara uliorasimishwa.

Mene amesema, itifaki hiyo inatarajiwa kushughulikia vikwazo ambavyo wanawake hukabiliana navyo wakati wa kufanya biashara barani Afrika.

Pia amesema, itaunda mazingira ambayo yataruhusu wanawake kutumia AfCFTA kupata masoko mengi, kuboresha ushindani wao, na kushiriki katika minyororo ya thamani ya kikanda.