Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Jumuiya ya SADC.


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Ndugu Doto James aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara na Kikosi kazi cha Mawaziri wanaohusika na Mtangamano wa Kiuchumi katika Jumuiya ya SADC kwa ngazi ya Makatibu Wakuu/Maafisa Waandamizi ulioanza leo tarehe 26  hadi 30 Julai 2021 kwa njia ya mtandao.

Aidha, katika muendelezo wa mkutano huo tarehe 30 Julai 2021, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania katika  Mkutano wa ngazi ya Mawaziri. Mkutano wa Mawaziri utahudhuriwa na  Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Viwanda, Biashara na Mtangamano wa Kiuchumi katika SADC.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utapokea taarifa na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji na Ujumuishaji wa Eneo Huru la Biashara la SADC (SADC FTA); Majadiliano ya Angola kuridhia Itifaki ya Biashara; Majadiliano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  kuridhia Itifaki ya Biashara; Ombi la Tanzania kuongezewa muda wa kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha katika bidhaa ya Sukari kutoka nchi za SADC; kujadili na kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru (NTBs);  utekelezaji wa Mradi wa masuala ya Biashara (Trade Related Facility);  Majadiliano ya Biashara ya Huduma ya SADC;  masuala ya Vikwazo vya Kiufundi vya Biashara (TBT); na Afya, Usalama wa Binadamu, Wanyama na Mimea (SPS).

Mkutano huu wa Jumuiya ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo nchi 12 katika ya 16 zimeshiriki kwa njia ya mtandao. Nchi zilizoshiriki ni pamoja na  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zimbabwe, Msumbiji, Malawi, Angola, Mauritius, Namibia, Botswana, Eswatin, na Zambia.