Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

PROFESA MKUMBO AWAASA TAA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA PAMOJA NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb) amewaagiza Wahasibu hapa nchini kutoa mchango katika kukuza na kuendeleza uwekezaji na biashara ili kutimiza kwa vitendo dira na Mpango wa Taifa wa maendeleo inayohimiza maendeleo ya viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini.

Mhe. Mkumbo ametoa agizo hilo tarehe 22 Julai, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 38 wa Wahasibu na Wakaguzi wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) huku akielezea mpango wa serikali katika kipengele cha kuendelea kuvutia uwekezaji.

"Serikali tumejizatiti katika kuhakikisha tunavutia uwekezaji wa nje, ili tuwe na mitaji mikubwa lengo likiwa ni kukuza pato la Taifa. Mkazo umetolewa katika eneo la kuvutia wawekezaji wa nje" alisema Profesa Mkumbo na kuongeza kuwa,

"Tunahitaji mitaji mikubwa na mitaji hiyo mikubwa ndio inayoingia moja kwa moja katika kujenga pato la Taifa"

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) amehoji juu ya hatua ambazo TAA zinachukua baada ya wahasibu kugundulika kufanya makosa kama njia kurekebisha kasoro na kuimarisha nidhamu.

"Wahasibu wenzetu wanafanya makosa na makosa yao yanajulikana hata wakaguzi huyaona na kuyaainisha makosa hayo, sisi kama wabunge tunajiuliza Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) mnachukua hatua gani" alisema Mhe. Hasunga.

Akielezea baadhi ya majukumu ya chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Rais wa chama hicho, CPA Peter Mwambuja amesema majukumu hayo ni pamoja na kuwashauri wafanyabiashara njia sahihi za kuwekeza, namna bora na nafuu za kutafuta mitaji, utafutaji wa masoko ya uhakika, kupunguza gharama za uendeshaji na kutoa ushauri katika maeneo mengine.

Mkutano huo umelenga kushirikisha uzoefu na masuala mbalimbali ya kitaaluma kwa Wahasibu na Wakaguzi pamoja na kupitia taarifa ya fedha kama ilivyopitiwa na Mkaguzi wa Hesabu, kupitia mpango mkakati wa chama hicho wa miaka mitano tukio ambalo litafuatiwa na zoezi la uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaongoza kwa kipindi cha miaka miwili kwa mujibu wa katiba ya TAA.