Wizara ya Viwanda na Biashara

Waziri wa Viwanda na Biashara

Hon. Innocent Lugha Bashungwa (MP)

Wasifu

Tamko la Waziri wa Viwanda Na Biashara kuhusu changamoto ya upatikanaji wa Sukari.


Imewekwa: 16th April, 2020

Serikali imewahakikishia watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari Tanzania hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile. Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa (Mb) ameyasema hayo Jijini Dodoma leo tarehe 16 Aprili 2020 wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari. Amesema kuwa kila mwaka serikali imekuwa makini katika kutathmini mahitaji ya sukari kwa wananchi kadhalika uwezo wa viwanda vya ndani katika uzalishaji. Bashungwa amesema ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na kirusi cha Corona. Ili kukabiliana na kadhia hiyo serikali imetoa vibali vya jumla ya Tani 40,000 kwa kampuni 4 za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza Tani 10,000. Waziri Bashungwa amesema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni Tani 9,990 na imeanza kutolea bandarini tangu jana jioni. Kadhalika tarehe 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya Tani 10,000. Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza jumla Tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku Tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini. Sambamba na hayo amesema kuwa wiki ya kwanza ya mwezi Mei Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza Tani 7,276 huku tarehe 15 Mei kampuni ya TPC itaingiza Tani 5,000 na Tarehe 30 Mei Tani 4,500 zitaingia nchini. Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema kuwa Wizara inatarajia kuomba nyongeza ya Tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020. Hata hivyo amesema kuwa Asilimia 80% ya sukari ambapo kwa mujibu wa Takwimu mahitaji ya sukari inayotumiwa majumbani ni kiasi cha Tani 470,000 ambapo kati ya hizo Tani 378,000 zinazalishwa nchini. Bashungwa amesema kuwa Hiyo ni hatua kubwa kwa nchi na serikali katika mkakati wa kuimarisha uchumi wa viwanda huku wawekezaji wengi wakiendelea na mchakato wa uongezaji tija na uwezo wa uzalishaji. Kadhalika wakulima wamekuwa na mtazamo mkubwa katika kuzalisha miwa kwa wingi ambayo wataipeleka katika viwanda vya kuchakata sukari na Katika kipindi cha hivi karibuni serikali itafikia uwezo mkubwa wa uzalishaji hivyo kuwa na ziada ya skari itakayouzwa nje ya nchi.

Hatimiliki © wizara ya viwanda na biashara 2020. Haki zote zimehifadhiwa.