Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA DHARURA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC)


Tanzania imezisisitiza Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kufanya uchambuzi wao wa kina wa Mkataba wa Ushirikiano baina ya Jumuiya Nchi za Afrika (AU) kabla ya kusaini Mkataba huo ili kuhakikisha maslahi ya nchi moja moja yanafikiwa bila kuathiri maslahi ya nchi nyingine, Mtangamano wa kikanda na Bara la Afrika, na umuhimu wa kuhusisha Jumuiya nyingine za kiuchumi barani Afrika.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akiongoza Ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 4-6 Oktoba 2021, katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (NJE), Mtumba.

Aidha, Ujumbe ulioongozwa na Waziri Mkumbo ulijumuisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbaruku Nasser Mbaruku, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo E. Longopa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina K. Shaaban ulitoa msisitizo huo  kwa lengo la kuja na mikakati maalumu ya kuiwezesha SADC kunufaika na fursa kupitia mpango unaopendekezwa wa NDICI na umuhimu wa maazimio ya Mkutano huo yakazingatiwa sanjari na jitihada nyingine zinazoendelea kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area=AfCFTA).

Mkutano huo ulilenga la kujadili Mkataba wa Ushirikiano baina ya SADC na Umoja wa Afrika, Pasifiki, na Karibeani (Organization of African, Carribean and Pacific States- OACPS), naUmoja wa Ulaya (European Union-EU); na Programu ya Maendeleo ya Ujirani na Ushirikiano wa Kimataifa (Neighborhood Development and International Cooperation Instrument – NDICI) ambapo nyaraka zilizopendekezwa ziliridhiwa na pande hizo mbili na kuongeza mahusiano mapya kati ya OACPS na EU.

Kupitia Mkutano huo, Nchi wanachama wa SADC wamekubaliana kuwa ipo haja ya kufanyia kazi haraka baadhi ya maeneo yanayohusu Mkataba husika kabla nchi hizo hazijafanya uamuzi ya kuridhia na kutekeleza Mkataba huo, kimsingi nchi hizo zimekubaliana kushirikiana na kuwa na msimamo wa pamoja katika kuliendeleza suala hilo na kuzingatia maslahi na juhudi zinazoendelea za mtangamano wa SADC na Bara la Afrika kwa ujumla.