Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA YAZINDUA NEMBO YA VIUNGO VINAVYOZALISHWA NCHINI.


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amezindua Nembo ya Viungo Tanzania (Tanzania Spices Label) ambayo itarahisisha na kuhakikisha bidhaa za viungo vya Tanzania zinatambulika kirahisi katika masoko mbalimbali ulimwenguni ikiwa ni hatua kubwa na muhimu sana katika kukuza mazao na bidhaa za mazao ya viungo nchini.

 

Uzinduzi huo umefanyika Julai 09, 2021 kwenye viwanja vya Maoneshoya Mwl. J. K. Nyerere (Saba saba) barabara ya kilwa Dar es salaam

 

Mhe. Kigahe amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mazao ya viungo vya chakula duniani na kuuza katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi,  takwimu zinaonesha kwa sasa tunazalisha aina 30 ya viungo hata hivyo kupitia mradi wa MARKUP tumejikita kuboresha na kuendeleza aina tano za viungo vya chakula ambavyo ni Karafuu, Mdalasini, Pilipili Manga, Iliki na Tangawizi.

 

Aidha, Mhe. Kigahe ameeleaza kuwa uanzishwaji wa Nembo ya viungo Tanzania itasaidia kutangaza bidhaa za viungo vya katika masoko mbalimbali  na kuwezesha kutambuliwa sokoni kirahisi na kuwaongezea wateja imani juu ya ubora wake pia kuitangaza nchi yetu kimataifa.

 

Mhe. Kigahe amemaliza kwa kutoa wito kwa Watanzania na kuziomba Taasisi na makampuni kuwekeza kwa kujenga viwanda vya kuongezea thamani mazao yetu ya viungo ili kuongeza tija na kipato kwa wakulima wetu na taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Doto James ameeleza kuwa katika ulimwengu wa masoko ya bidhaa kwa sasa watumiaji wanapenda kutumia bidhaa wanayoiamini na kuifahamu hivyo kama nchi ili tuweze kufanya vizuri masoko ya ndani na nje ya nchi inatubidi kuanza kukuza rajamu za bidhaa zetu “branding”, rajamu ni kitu muhimu sana katika kuboresha bidhaa na kuzifanya ziwe na thamani kubwa Pamoja na kujitetea pale panapokuwa hapana mtu wa kuitetea.

 

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade na Balozi Mteule Bw. Edwin Rutageruka amebainisha kuwa  Mamalaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania  Pamoja na majukumu mengine iliyopewa kisheria pia ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini zinatambuliwa na kuwa na rajamu “Brand” katika masoko ya ndani Pamoja na nje ya nchi, ili kuweza kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali sokoni rajamu ni suala muhimu sana hata hivyo rajamu ya bidhaa haiishii tu kutangaza bidhaa bali pia kutangaza nchi.