Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Habari

Uondoaji wa Kodi na Utoaji wa Ruzuku umeleta Nafuu katika Soko


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuondoa baadhi ya kodi na kutoa ruzuku kwenye mafuta ya petroli na dizeli imeleta nafuu kubwa kwenye bei za bidhaa sokoni.

Dkt.Kijaji ameyasema hayo Septemba 15, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya tathimini  ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini katika kipindi cha Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022.

"Hata hivyo, kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba hali ya upatikanaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwenye soko la dunia imeendelea kuimarika ambapo bei za bidhaa hizo zimeshuka na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa. Kutokana na hali hiyo, tunatarajia katika siku zijazo bei za bidhaa nchini zitaendelea kushuka na kuleta unafuu katika soko la ndani,"amefafanua Dkt.Kijaji.

Akiendelea kutoa taarifa ya tathimini, iliyofanywa katika kipindi cha mwezi Agosti 15 hadi Septemba 15, 2022, Dkt amebainisha ongezeko dogo la bei katika baadhi ya bidhaa za vyakula hususani mchele, mahindi, na maharage ambalo limetokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 uliosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao hayo. 

 Aidha Waziri Kijaji amesema Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufuatilia na kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wa kutoa taarifa za kila mwezi za mwenendo wa bei  nchini. 

Akifafanua upatikanaji wa taarifa hizo  amesema takwimu za bei za baadhi ya mazao ya chakula zinakusanywa kutoka kwenye masoko mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Wakusanya Taarifa za Masoko (Market Monitors). 

Vilevile amesema taarifa za bei za baadhi ya bidhaa muhimu kama vile bidhaa za vyakula, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine zinakusanywa kwa kutumia Maafisa Biashara wa  Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.

Waziri pia amebainisha kuwa, kila mwezi Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakusanya taarifa za bei kutoka kwenye masoko yaliyopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kukokotoa kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwezi husika. 

Amesema,bei za bidhaa kwa kila mkoa hupatikana kwa kukokotoa wastani wa bei za mazao na bidhaa hizo kutoka kwenye masoko yaliyopo kwenye mikoa hiyo.