Wizara ya Viwanda na Biashara

Waziri wa Viwanda na Biashara

Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe (MP)

Wasifu

UPATIKANAJI NA BEI ZA MAFUTA YA KULA NCHINI


Imewekwa: 26th January, 2021

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amesema hatasita kuwafutia leseni za biashara wafanyabiashara watakaoongeza bei ya mafuta ya kula nje ya ongezeko la bei halisia kutokana na bei ya soko la dunia. Waziri Mwambe alisema hayo akiongea na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji na bei ya mafuta ya kula leo tarehe 26 Januari 2021 katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha biashara (CBE) jijini Dodoma na kuongeza kuwa kwa sasa kuna mafuta ya kutosha yanayokidhi mahitaji ya mafuta ya tani 30,000 kwa mwezi kutokana na mafuta yaliyopakuliwa na meli mbili za mafuta hivi karibuni. Akiongea na waandishi hao, Mhe. Mwambe alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupunguza gharama na muda unaotumika katika upakuaji wa mafuta ya kula bandarini kwa wafanyabiashara wanaoagiza mafuta hayo nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya tani 365,000 kati ya tani 570,000 zinazohitajika kwa mwaka mzima ambapo mafuta yanayozalishwa ndani ya nchi ni tani 205,000 tu. Aidha, Waziri Mwambe amewasihi vijana kuunda vikundi na kuanzisha mashamba ya uzalishaji mazao ya mbegu zinazotoa mafuta kama vile michikichi, karanga, ufuta na alizeti ili kukidhi mahitaji ya malighafi za uzalishaji mafuta ya kula katika viwanda vipatavyo 771 ambavyo huzalisha asilimia 25 ya uwezo wake uliosimikwa. Vilevile, Mwambe alisema, Serikali kupitia agizo la Waziri Mkuu inawasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahamasisha wakulima kuzalisha mazao yanayotoa mbegu zinazozalisha mafuta ya kula kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya mafuta nchini na kupunguza uagiaji wa mafuta nje ya nchi. Mhe Mwambe pia aliielekeza Tume ya Ushindani (FCC) Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda kuendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya mafuta na kuhakikisha kuwa bei hizo zinafuata uhalisia.

Hatimiliki © wizara ya viwanda na biashara 2021. Haki zote zimehifadhiwa.