Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Kuhusu Wizara

Wizara ya Viwanda na Biashara ni moja kati ya Wizara za Kisekta nchini iliyoundwa kwa Tamko la Serikali Na.144 la tarehe 22 Aprili, 2016 ambalo lilifanyiwa mabadiliko tarehe 7 Oktoba, 2017. Wizara imebeba dhamana na jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali inayohusiana na uendelezaji wa viwanda vikubwa, vya kati, vidogo na vidogo sana; biashara kubwa na ndogo; kukuza na kutafuta fursa mpya za masoko ndani na nje ya nchi pamoja na kuendeleza ushirikiano wa biashara  kikanda na kimataifa. Hivyo, ina jukumu la kuhakikisha azma hiyo ya Serikali inafikiwa kwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa sera na sheria zinazoongoza maendeleo ya Sekta ya Viwanda na Biashara. Azma hiyo inalenga kujenga uchumi jumuishi na shirikishi unaochochewa na shughuli za viwanda ili kuleta maendeleo ya uchumi na maisha bora ya wananchi wake.

Wizara inatekeleza Sera, Sheria, Mikakati, programu na mipango mbalimbali ya kisekta kulingana na miongozo ya kitaifa kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020; na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26. Aidha, Wizara inatekeleza Mpango Mkakati wa 2021/2022 – 2025/2026 unaotoa mwelekeo wa sekta katika utekelezaji wa masuala ya msingi yaliyoanishwa katika Mipango ya Kitaifa, Kimataifa na Maelekezo ya Viongozi Wakuu wa nchi.

Wizara ya Viwanda na Biashara ina nafasi ya kipekee katika kutekeleza azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Malengo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ni: Kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika kuzalisha na kukuza teknolojia zinazohitajika; Kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira kwa kulenga kujenga viwanda vinavyochakata malighafi na hivyo kuwa na mnyororo mrefu wa thamani; na Kufungamanisha sekta nyingine na sekta ya viwanda (backward and forward linkage) ili kuipaisha nchi katika hatua ya juu zaidi kwani tayari imefikia katika kiwango cha uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.